Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa eneo la Mokomoni, wadi ya Mekenene wamemshtumu Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga kwa madai ya kutoweka mikakati ya kutosha kukabili visa vya uhalifu katika eneo hilo.

Wakihutubu siku ya Jumanne wakati wa mkutano, wakazi hao walidai kuwa kamishna Onunga amefeli pakubwa kwa kutoangazia suala hilo, hata baada yao kuwasilisha lalama zao afisini mwake.

"Hii sio mara ya kwanza sisi kuporwa mali na makundi ya uhalifu. Tunashangaa ni kwa nini afisi ya Kamishna Onunga haijachukua hatua za kuwatuma maafisa zaidi wa polisi katika eneo hili, kwa operesheni za usiku ili kuwakabili wahalifu,” alisema Jackson Magangi, msemaji wa wakaazi hao.

Wakazi hao aidha walitishia kuandamana kulalamikia ukosefu wa usalama iwapo kamishna Onunga hatochukua hatua za kuhakikisha kuwa hali hiyo inadhibitiwa.

"Tumechoshwa na hali hii ya kushambuliwa na kisha kuporwa mali yetu na wahalifu ikizingatiwa kwamba kamishna Onunga ana wajibu wa kutuhakikishia usalama. Iwapo hilo halitafanyika, tutafanya maandamano kulalamikia hali hii," alisema Magangi.

Hata hivyo, kamishna wa kaunti hiyo Josphine Onunga alithibitisha kupokea malalamishi ya wakaazi hao,na kuahidi kushughulikia hali hiyo kwa haraka.

"Tayari nishapokea malalamishi ya wakaazi wa Mokomoni na nimeweka juhudi za kuhakikisha maafisa wa polisi wa kutosha wametumwa katika eneo hilo ili kudumisha usalama," alisema Onunga.