Wakaazi wa kijiji cha Kabatini katika eneo bunge la Bahati, wamelalamikia ubovu wa barabara ya kutoka Maili Sita kwenda Kabatini.
Wakaazi hao wamemtaka mbunge wao Kimani Ngunjiri kuingilia kati na kuwezesha ukarabati wa barabara hiyo.
Wakaazi hao walisema kuwa ubovu wa barabara hiyo unawasababishia hasara kwani wanashindwa kuwasilisha maziwa na mazao mengine sokoni kutokana na gharama ya juu.
Wakizungumza siku ya Jumanne, wakiongozwa na Gilbert Ngesha, wakaazi hao ambao wengi wanajihusisha na kilimo walisema kuwa mazao yao yanaozea mashambani huku wakiuza mengine kwa bei duni.
"Sisi kama wakulima wa eneo la Kabatini tunapata hasara kubwa sana kutokana na kuharibika kwa barabara hii. Mazao yanaozea shambani kwa kuwa tumeshindwa kuyafikisha sokoni kutokana na gharama iliyopanda," alisema Ngesha.
Aliongeza, "Kutoka Maili Sita tulikuwa tukilipa shilingi hamsini lakini sasa tunalazimika kulipa kati ya shilingi sabini na mia moja."
Wilberforce Wanderi ambaye ni mwenyekiti wa wakulima wa Kabatini alimtaka Ngunjiri kutenga pesa katika hazina ya CDF kufadhili ukarabati wa barabara hiyo.
"Mbunge wetu anapaswa kutumia fedha za CDF kukarabati barabara hii la sivyo watu wa Maili Sita na maeneo jirani watakosa vyakula na maziwa," alisema Wanderi.