Wakazi katika eneo la Mwachamago iliyoko wilayani Mrima wanakoseshwa usingizi kwa kile wanachokitaja kama uvamizi wa wadudu hatari wa funza.
Wakizungumza na mwandishi huyu mnamo siku ya Jumapili katika eneo hilo, mamake Abdul anavyofahamika amesema kuwa wanawe hawaendi tena skuli kwa sababu hata kutembea kumekuwa taabu kutokana na wadudu hao ambao wamekita kambi kwenye sehemu za miguu yake.
Naye Mzee mwingine Hassan, ameunga mkono matamshi ya mama huyo na kusema kuwa funza hao wamekuwa kikwazo kwa maisha yao ya kila siku na kuiomba serikali ya kaunti ya Mombasa kuwapa dawa za kuwaondoa kabisa wadudu hao.
"Japo kuwa tunajitahidi kufanya usafi, mazingira yetu pia ni duni ikizingatiwa kuwa watu wasiojulikana hubeba taka taka na kuja kuzitupa huku kwetu magwangwani. Hatuelewi kwa nini inakuwa hivi," alilalamika mama mwingine mwuzaji samaki.
Tatizo hili la funza linafwatia miezi kadhaa baada ya wakazi hao kulalamikia kero la kunguni ambao pia kwa sasa wamewakumbatia kama sehemu ya maisha yao huku wakidai kuwa kaunti imepuuza kilio chao cha msaada.