Mwanasiasa katika eneo bunge la Borabu kaunti ya Nyamira Yobesh Nyandoro Kambi amewahimiza wakaazi wa kaunti za Kisii na Nyamira ambao wamefikisha umri wa miaka 18 kujiandikisha kupata vitambulisho ili kubadilisha uongozi na kuleta maendeleo ifikapo mwaka wa 2017.
Kulingana naye viongozi wengi walio katika mamlaka hawafanyi maendeleo jinsi inavyohitajika na kusema wakati umetimia wa kubadilisha uongozi ili maendeleo kushuhudiwa katika eneo la Kisii kupitia viongozi walio tayari kufanya maendeleo.
Akizungumza siku ya Jumapili katika uwanja wa Nyatieko eneo bunge la Kitutu Chache Kusini wakati wa finali za kombe la mtangazaji ambaye pia ni mcheshi wa kituo cha radio Egesa Fm Petronira Getena zilikuwa zinachezwa, Nyandoro alikiri kuwa itakuwa vigumu katika uchaguzi ujao ikiwa mkaazi hana silaha ya kitambulisho ili kumchagua kiongozi wa maendeleo.
Aidha, Nyandoro aliwashauri wale ambao tayari wamechukua vitambulisho hivyo kuhakikisha wamejiandikisha kama wapiga kura ili wasikae na vitambulisho ambavyo haviwezi kuwasaidia na kujaribu kila wawezalo kuhakikisha wamepata kadi za kupiga kura.
“Yeyote amefikisha umri wa miaka 18 naomba kwa unyenyekevu ujiandikishe kuchukua kitambulisho na kadi ya kura ili tubadilishe uongozi ifikapo mwaka wa 2017 kwani imeonekana viongozi walio mamlakani hawako tayari kufanya mendeleo kikamilifu,” alisema mwanasiasa Nyandoro.
“Ikifika uchaguzi ujao huenda iwe vigumu kumchagua kiongozi wa maendeleo maana huna kadi ya kumchagua na kitambulisho kama silaha sharti tuungane pamoja ili tupate viongozi wa maendeleo,” aliongeza Nyandoro.
Nyandoro alitangaza kukiwania kiti cha ubunge katika eneo bunge la Borabu tena ifikapo 2017.