Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wa eneo la Chepilat, eneo bunge la Borabu, wametishia kuandamana ikiwa hawataimarishiwa usalama katika eneo hilo.

Wakazi hao walisema kuwa kuna ongezeko la majambazi wanaoendelea kuwasumbua.

Haya yanajiri baada ya dereva mmoja wa eneo hilo kuvamiwa na washukiwa wa ujambazi wiki jana alipokuwa anaelekea kazini na kujeruhiwa. Dereva huyo anaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Litein.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika eneo la Chepilat, wakazi hao, wakiongozwa na Joshua Morara, walitishia kuandamna ikiwa hawataimarishiwa usalama.

Wakazi hao waliomba maafisa wa polisi kufanya uchungunzi na kubani washukiwa hao wa ujambazi ambao wanaendelea kufanya mashambulizi na kuwatia mbaroni.

“Tunaomba maafisa wa polisi waweze kutuimarishia usalama wetu hapa Chepilat maana tunahofia maisha yetu,” alisema Morara.

Aliongeza, “Genge hilo la wezi limezoea kuwashambulia wakazi saa kumi na moja asubuhi wanapokua wakienda kazini. Tayari tumempoteza dereva mmoja na mwengine yuko hospitalini akipokea matibabu.”

Wakazi hao walisema majambazi hao walikuwa wakifanya mashambulizi katika sehemu za Keroka na Kijauri lakini kwa sasa wamehamia eneo la Chepilat.