Wakazi wa Kinungi katika kaunti ndogo ya Naivasha walifanya maandamano kulalamikia ongezeko la visa vya ajali.
Wakazi hao waliokua na gadhabu walifunga barabara kuu ya Nairobi-Nakuru siku ya Alhamisi na kutatiza shughuli za uchukuzi katika barabara hiyo.
Wakazi hao waliitaka serikali kuwawekea matuta katika barabara hiyo kama njia moja ya kudhibiti visa vya ajali.
Walisema eneo la Kinungi limekumbwa na visa vingi vya ajali za barabarani, ikiwemo ajali moja ambapo mtoto wa umri wa miaka tano aligongwa na gari na kufa papo hapo.
Waandamanaji hao walichoma magurudumu ya magari na kuweka mawe katika barabara hiyo hatua iliyowalazimisha maafisa wa polisi kuingilia kati.
William Kinyua, mkazi wa sehemu hiyo alishtumu polisi kwa kuwarushia vitoa machozi wakati wa maandamano hayo.
"Hapa kila mwezi nilazima mtu agongwe na gari ndiposa tumeamua kuandamana. Lakini ninashtumu polisi kwa kuturushia vitoa machozi ilhali tunatafuta haki na hatujaharibu kitu cha mtu," alisema Kinywa.