Hatua ya idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa kufwatilia kwa karibu njama za wanamgambo wa kundi la al-Shabab la kuwasajili vijana wa kurandaranda mtaani imetajwa kusaidia kuimarisha usalama.
Kulingana na kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni, Maxwell Masai, hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwanusuru vijana kutokana na kujiunga na kundi hilo.
Masai alisema kwamba ni jukumu la kila mkazi kushirikiana na maafisa wa usalama kutibua njama hizo.
Akihutubia mkutano wa kiusalama wa wakazi wa eneo la Kisauni, siku ya Jumatatu, Masai alisema kwamba lazima mashirika ya kijamii, viongozi wa kidini na wanaharakati wa maswala ya kiusalama kuungana kuwashauri vijana kuepukana na ugaidi kabla vijana hao kuangamizwa.
"Tafadhili wakazi wa eneo hili tushirikiane na maafisa wa polisi, mashirika ya kijamii, viongozi wa kidini na wanaharakati wa maswala ya kiusalama ili tuweze kutibua njama za magaidi kabla hawajaangamiza vijana wetu. Mbinu wanazotumia kwa sasa ya kuwasajili vijana wa kurandaranda mtaani inahatarisha maisha ya wakazi,” alisema Masai.
Masai aliwahimiza vijana kutokubali kushawishiwa vibaya na baadhi ya watu wasio wafahamu vyema ili kuona kwamba wanatimiza ndoto zao za kuzisaidia familia zao katika siku za usioni.
Kuali ya Kiongozi huyo wa vijana imejiri siku chache baada ya idara ya usalama katika kaunti hiyo kutangaza kuchunguza baadhi ya makundi yanayoshukiwa kuwa wafuasi wa kundi la al-Shabab wanaowasajili vijana wa kurandaranda mtaani.