Wakazi wa Mombasa wamepongeza mpango wa kujenga gereza maalumu la urekebishaji tabia kwa wafungwa wenye misimamo mikali nchini.
Kwenye mahojiano siku Jumatano na mwandishi huyu, wakazi wa Kisauni, wakiongozwa na Tomy Simba, walisema kuwa gereza hilo litawasaidia pakubwa vijana wenye misimamo mikali na kuwatenga na wafungwa wengine wasio na misimamo hiyo.
Aidha, wakazi hao wameitaka serikali kutafuta mbinu mbadala ya kukabiliana na vijana wenye itikadi kali za kidini kote nchini.
Siku ya Jumanne, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza mipango ya serikali kujenga kituo kipya cha urekebishaji tabia ili kuwazuia wafungwa wenye misimamo mikali.
Kenyatta alisema kuwa jela hiyo itajengwa ili kuwatengenisha wafungwa wanaotuhimiwa kwa makosa ya misimamo mikali, kama njia moja ya kuzuia wafungwa hao kusambaza itikadi hizo kwa Wakenya wengine.
Rais Kenyatta alisema serikali imejitolea kuwazuilia wahalifu katika mazingira yatakayowawezesha kurekebisha tabia ili waingiliane na jamii na kutoa mchango ufaao kwa jamii.
Rais alisema kuwa kurekebisha tabia ya wahalifu kunahitaji watu waliojitolea mhanga ili kuutumikia umma kwa kuwatunza katika hali ifaayo.
Rais aliyazungumza haya wakati wa kufuzu kwa makurutu zaidi ya 2,300 wa askari gereza katika chuo cha mafunzo cha Ruiru kilichoko kaunti ya Kiambu.