Wakazi kaunti ya Mombasa wamepongeza hatua ya kuondolewa mashtaka ya uuzaji wa ardhi ya soko la Mwembe Tayari yaliyokuwa yanamkabili Gavana wa Mombasa Hassan Joho.
Wakiongozwa na mkazi wa eneo la Mshomoroni Wyclif Okumu, wakazi hao wamesema kuwa hatua hiyo ni dhihirisho tosha kuwa Joho si kiongozi bepari.
Siku ya Alhamisi, kiongozi wa mashataka ya umma Keriako Tobiko alimwondolea Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho madai ya kupeana soko la Mwembe Tayari kwa mfanyakazi wa kibinafsi kinyume cha sheria.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Tobiko alieleza kwamba kulingana na ripoti za serikali, soko hilo lilitolewa kinyume cha sheria mwaka 1996 na baraza la manispaa ya Mombasa.
Soko hilo lilikodishwa kwa mda wa miaka 99 na kupewa Mohammed Abdullah na Abdulhakim Abdullah kwa sheria za serikali za wilaya.
Tobiko alisema hakuna ushahidi kwamba Joho ama serikali ya Kaunti ya Mombasa imehusika katika kukodishwa kwa soko hilo.