Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa Kaunti ya Nyamira wana kila sababu ya kutabasamu baada ya wataalamu kutoka marekani kuzuru kaunti hiyo kwa siku tano, ili kuwapa wakazi mafunzo kuhusiana na mbinu mwafaka za kuthibiti mikasa.

Akihutubu wakati wa kuwapokea rasmi wataalamu hao ofisini mwake siku ya Jumatatu, Gavana wa Nyamira John Nyagarama aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kutoishtumu serikali yake kuhusiana na ukosefu wa magari ya kuzima moto, ila kushirikiana na serikali hiyo kuthibiti mikasa ya aina hiyo.

"Ni himizo langu kwa wakazi wa kaunti hii kuasi tabia ya kuishtumu serikali kila mara mikasa ya moto inapotokea, kwa maana twahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kuthibiti visa hivyo," alisema Nyagarama.

Nyagarama aidha aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kuripoti visa vya mikasa ya moto kwa mapema ili kusaidia idara husika kushughulikia mikasa hiyo kwa haraka.

"Ili serikali iwe na uwezo wa kuthibiti visa vya mikasa kwa haraka, sharti wananchi watoe ripoti kuhusu visa hivyo kwa haraka ili kuiwezesha serikali kushughulika mapema, kabla mikasa hiyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mali," aliongezea Nyagarama.