Mkurugenzi wa matibabu katika Kaunti ya Nyamira Dkt Jack Magara amesema kuwa visa vya ugonjwa wa kisukari miongoni mwa wakazi wa kaunti hiyo vimeongezeka.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia wanahabari siku ya Ijumaa kwenye uwanja wa Shule ya msingi ya Nyamira, wakazi walipokuwa wamejitokeza kupimwa ugonjwa huo, Magara alisema kuwa watu wengi ni waathiriwa wa ugonjwa wa sukari lakini hawana ufahamu.

Daktari huyo alisema kuwa sharti wananchi wajitokeze kupimwa ili waweze kupata matibabu kwa haraka.

"Wakazi wengi wa Nyamira ni waathiriwa wa ugonjwa wa kisukari ila tu ni kwamba wengi wao hawana ufahamu kwasababu hawajitokezi kupimwa. Ningependa kuwahimiza wajitokeze kupimwa iwapo wana ugonjwa huo ili wapate matibabu ya mapema yatakayo wawezesha kuthibiti ugonjwa huo," alisema Magara.

Magara alisema kuwa mazoea yakula vyakula visivyo na virutubishi muhimu, na kutofanya mazoezi yanachangia wakazi kuugua ugonjwa wa kisukari.

"Watu wengi wana mazoea ya kula vyakula visivyo na virutubishi muhimu na kutofanya mazoezi mara kwa mara hali inayo waweka kwenye hatari yakupata ugonjwa wa sukari. Nawahimiza wakazi wawe na mazoea yakula vyakula vilivyo na virutubishi muhimu na pia kufanya mazoezi ili kuepuka ugonjwa huu,” alisema Magara.