Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi Pwani wametakiwa kutoa ripoti kwa vyombo vya usalama kuhusu washukiwa wa ugaidi wakiwemo wale wa kundi la al-Shabaab.

Kauli hii imetolewa na Meja Hinzano Mumbo, aliyeongoza mazishi ya mwanajeshi Rophas Amani Lwembe, aliyeuawa huko Somalia mwezi uliopita.

Meja Hinzano alisema magaidi wangali humu nchini na wanaendelea kujisajili kila uchao na kuwataka raia kushirikiana na idara ya usalama katika kupiga vita ugaidi nchini.

Marehemu Rophas Amani Lwembe alikuwa na umri wa miaka 26 na alijiunga na kikosi cha KDF miaka mitano iliyopita.

Itakumbukwa kuwa baadhi ya wanasiasa nchini wameitaka serikali kuliondoa jeshi lake nchini Somali baada ya wanajeshi wa KDF kuvamiwa na kuuawa nchini Somali mwezi uliopita.

Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale aliitaka serikali kuliondoa jeshi la KDF nchini Somlia ili visa vya uvamizi wa kigaidi kupungua nchini.

Seneta huyo lisema kudorora kwa sekta ya utalii kumechangiwa na ukosefu wa usalama nchini.

Khalwale alisema kuwa serikali sharti iondoe jeshi la KDF kutoka Somalia, na kuliweka mpakani mwa taifa ili kuliwezesha kupambana na magaidi.

Seneta huyo alisisitiza kuwa kuondolewa kwa jeshi hilo nchini Somalia kutamaliza mashambulizi yanayotekelezwa humu nchini na wafuasi wa al-Shabaab, sawia na kukomesha maafa yanayowakumba wanajeshi wa Kenya.

Hadi sasa, serikali haijaweka bayana idadi kamili ya wanajeshi waliouawa kwenye shambulizi hilo lililotokea huko El Adde, Somalia mnamo mwezi Januari.