Share news tips with us here at Hivisasa

Polisi eneo la Kaloleni, Machakos walikuwa na kibarua kigumu cha kuwafurusha waandamanaji waliokuwa wamefunga barabara ya kutoka Machakos kwenda Wote katika eneo la Katoloni. 

Watu hao walikuwa wameandamana kutokana na ongezeko la visa vya ajali za barabarani eneo hilo.

Hii ni baada ya mwanamune mmoja wa umri wa makamo kupoteza maisha yake Jumamose usiku huku akipata matibabu katika hospitali ya Machakos baada ya kugongwa na gari aina ya maruti, na dereva kutoroka baada ya ajali hiyo. 

Waandamanaji hao, wakiongozwa na Francis Musembi ambaye ni mzazi wa mwanamume aliyeaga dunia baada ya ajali walielezea kuwa walifunga barabara ili kutengeneza tuta kama njia mojawapo ya kuzuia ajali hizo.

"Jana usiku nmempoteza mwanangu na singetaka mtu mwingine aage dunia kutokana na ajali na hivyo tukajitokeza kuweka tuta katika eneo hili ili kupunguza kasi ya magari,"alisema Musembi. 

Waandamanaji hao walielezea kuwa ambulensi ilifika imechelewa baada ya ajali hiyo, na waliamini kuwa mwanamme huyo hangekufa iwapo ambulenai ingefika mapema.