Kampuni ya kusambaza nguvu za umeme nchini KPLC imelaumiwa vikali kwa kuwalipisha wakazi gharama ya stima ambayo ni ya juu zaidi kuliko ile waliyoitumia.
Hii ni baada ya idadi kubwa ya wakazi wa kaunti ya Kisii kupokea gharama ya juu katika mwezi wa kwanza, jambo ambalo wamelikashifu vikali.
Wakazi hao walijumuika siku ya Alhamisi katika ofisi za kampunu hiyo ya KPLC tawi la Kisii kupeleka malalamishi yao na kutaka kuhudumiwa vyema.
“Mimi mwenyewe nimekuwa nikilipa shilling 200 kila mwezi, lakini mwezi huu wa kwanza nilipokea gharama ya 10,000 mpaka nikashindwa ni nini kinaendelea, inaonekana kampuni hii imeanza kutuchezea, tunahitaji kuelezwa kwa nini haya yanafanyika,”alisema Patrick Masiita, mkazi.
“Ata mimi nilihitajika kulipa 5,000, na nilishangazwa maana sijawai kulipa zaidi ya shillingi 150 kila mwezi, tunataka kuelezwa kwa nini hayo yanafanyika,” alisema Joshua Misati, mkazi mwingine.
Aidha, wakazi hao walisema maafisa wale wa kusoma mita za wakazi mwezi wa kwanza hawakupita katika nyumba zao.
Mwenyekiti wa kampuni hiyo tawi la Nyanza kusini David Mogambi alipokea malalamishi ya wakazi hao na kuahidi kutafuta suluhu halisi na kusema hilo halitarudiwa tena.