Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa eneo la Mang’u katika kaunti ndogo ya Rongai, kaunti ya Nakuru, wamelalamikia ukosefu wa maji katika eneo hilo.

Wakizungumza wakati wa mkutano na Mbunge Wa Rongai Raymond Moi, katika eneo la Mang'u siku ya Alhamisi, wakazi hao, wakiwakilishwa na Alfred Mwanzia, walisema wamekuwa wakilazimika kununua maji kwa muda mrefu sasa.

"Tunalazimika kununua maji kutoka kwa bwawa la Makiki kwa shilingi ishirini kwa kila mtungi wa lita ishirini, kwa hivyo tunakuomba wewe kama mbunge wetu, uweze kututalia kero la ukosefu wa maji," alisema Mwanzia.

Walisema kuwa shida hiyo imekuwepo kwa muda wa zaidi ya miaka saba sasa, na hawajapata usaidizi wowote licha ya kupokea ahadi kutoka kwa viongozi waliowachagua.

Walisema kwamba, licha ya kuchagua kamati ambayo itasaidia kutatua shida mbalimbali katika eneo hilo, bado hakuna dalili zozote za kusaidika.

Hata hivyo, Moi alikanusha swala hilo akisema kwamba shida ya maji kwenye eneo la Mang'u na hata Rongai kwa jumla, itafikia kikomo kwani serikali ya kitaifa imeanzisha mradi wa Maji ya bwawa la Chemususu lililoko Baringo, maji ambayo yatafaidi hata wakazi wa mji wa Nakuru katika kipindi kifupi kijacho.