Wakazi katika baadhi ya mitaa ya Kaunti ya Mombasa wanaitaka serikali pamoja na idara ya kushughulikia maswala ya watoto kufuatilia kwa makini maadili ya watoto eneo hilo.
Hii ni baada ya madai kuibuka kwamba watoto kutoka maeneo kadhaa ya kaunti hiyo wanajihusisha na tabia ya unywaji pombe, jambo ambalo wenyeji wa eneo hilo wanasema linapotosha maadili.
Wenyeji wa eneo la Mariakani wanalalamikia tabia hiyo wakisema watoto katika mitaa hiyo wana mazoea ya kutembelea vilabu vya kuuza pombe na kunywa.
Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, wakazi hao wanasema tabia hiyo imekithiri mno.
“Hawa ni watoto wadogo hata wengine wanafaa kwenda shuleni lakini pombe inawaharibu,” alisema mkazi mmoja.
Hata hivyo, wamewalaumu wazazi kwa kutowalinda watoto wao na kuwafunza maadili ndiposa wakajihusisha na tabia hiyo.
Pombe hiyo ambayo wakazi wanasema ni 'chang’aa' na ambayo imetajwa kuwa hatari imekuwa ikiuzwa eneo hilo kwa muda bila hatua yoyote kuchukuliwa.
Hapo awali, kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa aliwaonya wazazi kwa kutozingatia maadili ya watoto wao, huku akiwaonya watoto wa shule dhidi ya kuhudhuria sherehe za usiku maarufu kama kesha na kuwataka machifu katika kaunti hiyo kuwajibika.