Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa eneo la kaunti ndogo ya Molo wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kaunti ya Nakuru kupitia wizara ya mazingira kuzindua mradi utakaohakikisha vyoo vipya vimejengwa kama njia mojawapo ya kuimarisha afya ya wananchi.

Akizungumza na wanahabari siku ya jumatano katika eneo la Casino, kaunti ndogo ya Molo ambapo alizindua mradi wa kutengeneza vyoo vipya eneo hilo, waziri wa mazingira wa kaunti ya Nakuru Richard Rop ameelezea kuwa serikali ya kaunti tayari imetenga pesa zitakazotumika katika kujenga vyoo hivyo almaaruafu vyoo vya Safisan.

"Kaunti ya Nakuru itahakikisha kuwa maisha ya kila mmoja haitatarishwi na kuwa mnaishi kwa mazingira mema. Hii ndiyo maana tumetenga milioni nne ambazo zitatusaidia katika ukarabati wa hivi vyoo vipya," Rop alielezea.

Waziri huyo ambaye pia aliambatana na maafisa wengine katika wizara yake pia ameelezea kuwa watahakikisha mradi huo unafikia pia maeneo mengine katika kaunti hiyo wakishirikiana nashirika ya maji ya water service trust funds kupitia NARUWASCO.

"Shirikika la NARUWASCO limeahidi kutoa shilingi elfu ishirini kwa kila choo kipya kitakachijengwa pamoja na shilingi elfu kumi na tano kwa kila choo kitakachokarabatiwa. Lengo letu ni kudumisha ubora wa mazingira ili tuepuke magonjwa yanayochangiwa na mazingira duni," aliongezea Rop.

Mradi huo wa Safisan utaanza rasmi mwezi Januari mwaka ujao.