Kufuatia kisa cha mtoto wa miaka kumi kupigwa na nyaya za umeme na kuaga dunia, wakazi kutoka eneo la Shika Adabu wamelitaka shirika la umeme nchini KPLC kuchukua hatua ya kurekebisha nyaya ambazo wanadai zimening’inia baada ya kutingishwa na mawimbi na upepo mkali ambao umesababishwa na mvua kubwa ambayo inaendelea.
Wakazi hao wametoa ghadhabu yao kwa kusema kuwa shirika hilo limezembea kwa kutowajibikia maswala ya wakazi, hata baada ya lalama nyingi kuwa baadhi ya nyaya zimekatika na zinahitaji kurekebishwa ili kuzuia maafa nyakati za mvua hii nyingi inayoendelea kwenye maeneo mengi eneo la Pwani.
Kupitia kwa mama Fatma Hassan, ambaye aliongoza wenzake kutoa lalama hizo siku ya Jumatatu, wakazi hao walisema kuwa hatua za haraka zinafaa kuchukuliwa kuangalia si tu eneo hilo, bali sehemu ambazo mvua hiyo imenyesha ili kuziba mianya ya majanga kuchipuka.
Walipendekeza vile vile kuwa shirika hilo kufanya juhudi za kuwaelimisha wananchi jinsi ya kukabiliana na athari za sitima, na ni vipi wanaweza kujiepusha na hatari ambayo zinawakodolea macho ikizingatiwa kuwa bado kuna mafuriko na maji ya mvua yamejenga vidimbwi kwenye makazi.
Aidha wakazi hao waliomba serikali ya Kaunti ya Mombasa kuharakisha miradi na kutimiza ahadi walizotoa mapema kabla ya kuanza kwa mvua ya El Nino, na kushangaa ni vipi mamilioni ya pesa ammbazo zilitengwa ili kushughulikia athari ambazo zitasababishwa na mvua hiyo.