Maafisa wa polisi wamekuwa wakipiga doria katika eneo la Shika Adabu ambapo wakaazi wanadai kusumbuliwa na hata kupigwa na askari hao ambao wanaendelea kutafuta wahalifu wa genge lililompiga risasi askari huyo na kumuua.
Hii ni kufuatia kuuliwa kwa mmoja wa maafisa wa polisi mapema wiki hii.
Wakazi hao wamedai kuwa baadhi ya maafisa wa polisi wamekuwa na mtindo wa kuwashika wakazi hata bila kuwa na ushahidi tangu kushambuliwa kwa askari huyo huku wakisema kuwa polisi wanaingia nyumba za watu kwa lazima wakitafuta bunduki.
Kwenye mahojiano siku ya Ijumaa George Gondi ambaye ni mhudumu wa magari ya abiria anasema kuwa kwa siku tano sasa amejiepusha na kuenda kwenye shughuli yake ya kila siku ya kuhudumia abiria kwa kuogopa kuhangaishwa na maafisa hao wa polisi ambao wanaendelea kuwadhulumu wakazi kwa kisingizio cha kuwatafuta waliohusika.
“Hata ukitembea kutoka hapa hadi Likoni hasa nyakati za jioni hamna watu wanaotembea barabarani kwa sababu wameogopa kushikwa na unaelewa maafisa wa polisi wanaweza kukushika na kukusingizia chochote ilhali hauna kosa hata kidogo, hiyo sababu watu wanataka serikali kuu iingilie suala hilo ili kuleta suluhu la haraka,” alisema Gondi.
Wengine ambao waliongea na mwandishi habari huyo ni baadhi ya wauzaji wa bidhaa za rejareja ambao walisema kuwa wamekuwa na uoga wa kuuza bidhaa zao kwa kuogopa kushikwa na polisi.
Afisaa huyo wa polisi alipigwa risasi wiki hii na majambazi wanaodaiwa kuwa na nia ya kuiba katika eneo la Check-Point Shika Adabu.