Naibu kamishna katika kaunti ndogo ya Nakuru ametaja ukosefu wa uzalendo miongoni mwa baadhi ya wananchi kama chanzo cha maovu humu nchini.
Thomas Sankei, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati andalizi ya sherehe za maadhimisho ya sikukuu ya Jamuhuri katika Kaunti ya Nakuru, amewataka Wakenya kutilia maanani siku hiyo na kujumuika pamoja ili kuonyesha umoja na utangamano.
Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Alhamisi, Sankei aliwataka wakazi wa Nakuru pamoja na Wakenya kwa jumla kujitokeza Siku ya Jumamosi katika uwanja wa afraha wakati wa maadhimisho hayo.
Aidha, Sankei alisema kuwa kukiwa na utangamamo, visa vya uvunjaji wa sheria, na uhalifu mwingine vitazikwa katika kaburi la sahau.
Akizungumzia swala la usalama, Sankei alisema kuwa vyombo vya usalama viko imara kuhakikisha kwamba kila kitu ki shwari, kutokana na idadi kubwa ya watu kuzuru mji huo wa Nakuru.
Aliwahimiza wakazi katika eneo hilo kukumbatia mpango wa Nyumba Kumi na kushirikiana na maafisa wa polisi kwa kupiga ripoti, pale wanaposhuku mtu au kitu chochote kinachoweza kuhatarisha maisha.