Huku shule zikifunguliwa jumatatu kwa muhula wa kwanza kote nchini, wawakilishi wa wadi ya Nyamira wameombwa kufadhili shule na vitabu vya kusoma na kushirikiana kutafuta njia ya kuhakikisha viwango vya elimu vimeinuka katika eneo hilo.
Wito huo ulitolewa baada ya baadhi ya shule kufanya vibaya katika mtihani wa darasa la nane, matokeo ambayo yalitangazwa wiki jana kwa kaunti hiyo
Wakizungumza na waandishi wa habari jumapili katika eneo la Rigoma, bunge la Kitutu Masaba, wakazi wengi waliwaomba wawakilishi wadi kutoa ufadhili wa vitabu vya kusoma kwa shule na pia kushirikiana kutafuta mbinu ya kuinua viwango vya elimu katika shule za msingi na za upili.
Kulingana na wakazi hao, viwango vya elimu katika kaunti hiyo vinazidi kudorora katika baadhi za shule na kwamba kuna haja ya viongozi kushirikiana pamoja na kutafuta mbinu ya kuinua elimu.
“Tunaomba viongozi wetu hasua wawakilishi wadi kutoa ufadhili wa vitabu vya kusoma kwa shule zote na kushirikiana kuinua viwango vya elimu,”alisema Omwenga Kennedy.
Aidha, wawakilishi wadi waliombwa kuhakikisha kila shule iko na idadi ya walimu ya kutosha na kusema kuwa ikiwa walimu hawatoshi kwa shule hizo waombe serikali ya kitaifa kuongeza walimu kwa shule hizo .
“Tunaomba serikali kuongeza walimu mshahara kwa sababu huenda kile kinachangia elimu kudorora ni vile serikali haitaki kuongeza walimu mshahara wao,na walimu waajiriwe watoshe katika shule zote,” alisema Beatrice Achoki mkazi pia mzazi