Wakimbizi 539 kutoka eneo la Baringo wameitaka serikali kuwalipa fidia kabla ya mpango wa kulipa wakimbizi fidia kukamilika.
Wakiongea mjini Nakuru Jumatatu wakimbizi hao wamesema kuwa tangu zoezi la mpango rudi nyumbani kung’oa nanga baada ya mzozo wa vita vya baada ya uchaguzi mnamo 2007/2008, wao wamenufaika na shilingi 10,000 pekee.
Kwa sasa wameitaka serikali kufanya ujasiri na kuwashugulikia kama wakimbizi wengine nchini wanapofidia waadhiriwa.
“Baringo kuna IDPS walioadhiriwa na vita vya baada ya uchaguzi, na ni 539. Serikali ilitwambia turudi nyumbani, wale ambao hawakuweza walienda kwa marafiki zao. Sisi ni wakimbizi kama wengine, lakini wakati wao wanafidiwa, sisi tulipata shilingi elfu 10 pekee. Tunataka pia fidia,” alisema mwenyekiti wao samwel Marijor.
Kulingana na mwenyekiti wa wazee kutoka jamii za eneo la bonde la ufa Gilbert Kabage, wakimbizi hao wamekuwa wakifanya ziara katika afisi nyingi nchini huku wakikosa kupata afueni.
Haya yanajiri wiki moja tu baada ya wakimbizi 200 kutoka eneo la Mau Summit kufanya maandamano wakidai wanataka pia kulipwa fidia.
“Tunaelekea katika ofisi ya mratibu mkuu wa eneo la bonde la ufa hapa Nakuru, na kutafuta wawakilishi wengine ambao watatusaidia kuwasiliana na serikali ya Uhuru Kenyatta na naibu wake William ruto ili kilio chetu kisikike,” alisema.