Zaidi ya wakimbizi elfu 10 wa ndani kwa ndani wamelaumu mchakato wa serikali kuu kuwapa makao bila ya kutekeleza sera zilizowekwa katika sheria ya watu waliofurushwa kwao.
Wakiongea mjini Nakuru Jumapili na mwandishi huyu, wakimbizi hao waliitaka wizara ya mipango maalum kutekeleza sheria hiyo iliyopitishwa na serikali ya muungano mnamo Desemba mwaka wa 2012 ili kuwashugulikia wakimbizi.
Mkimbizi mmoja kutoka Nakuru, Peter Tenna, alisema kwamba haitawezekana kwa fedha kutengwa kwenye bajeti bila ya kuwa na sera dhabiti zitakazohakikisha kwamba kuna afisa mkuu wa fedha atakayesimamia utoaji wa fedha hizo.
Wakimbizi hao walisema kwamba haki zao kama wakimbizi zinakiukwa wakati wanalazimishwa kutia saini mikataba ya kupokea pesa kama fidia, ilhali kulingana na sheria hiyo wanapaswa kufidiwa kwa kupewa vipande vya ardhi.
Walilaumu maafisa wa ngazi ya juu serikalini kwa kuhitilafiana na mchakato wa kufidiwa kwa wakimbizi nchini, hitilafu ambazo wanasema zimesababisha kutumiwa vibaya kwa shilingi bilioni 15, swala linaloendelea kuchunguzwa na kamati spesheli ya seneti pamoja na tume ya EACC.