Wafugaji wa ngombe wa maziwa katika wadi ya Kiamaina watanufaika na kiwanda cha kuhifadhi maziwa kitakachojengwa katika eneo hilo kwa ufadhili wa hazina ya maendeleo bunge la Bahati.
Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, alisema kuwa tayari mipango ya kujenga kiwanda hicho imo mbioni.
Akizungumza Jumamosi wakati wa siku ya wakulima katika eneo la Maili Sita, Ngunjiri alisema kuwa kiwanda hicho kitawasaidia wakulima kuhifadhi maziwa yao ili yasiharibike.
"Tunajua hapa kuna wakulima wengi sana ambao wanazalisha maziwa na wanapata shida ya kuweka maziwa yao na ndio maana tumeamua kujenga kiwanda hapa ili wapate kusema maziwa yao yasiharibike,"akasema Ngunjiri.
Aidha mbunge huyo aliwataka wakulima kuboresha mbinu zao za ukulima ili kuboresha uzalishaji wa maziwa.
"Kama wakulima wanaweza kuzingatia mbinu bora za kilimo basi tunaweza kupata faida kubwa sana kwa sababu maziwa yatakuwa mengi na pesa tutapanga,"akasema.
Ngunjiri aliongeza kuwa pia atafadhili ujenzi wa josho la kuoshea ngombe ili wakulima wapate mahali pa kuwatibu ngombe wao.
"Pia tutajenga cattle dip hapa ili mweze kuwaosha hawa ngombe wenu kwa dawa kila mara ili kuwakinga na wagonjwa,"akasema.
Hafla hiyo iliandaliwa na muungano wa wakulima wa Bahati ili kuwapa wakulima mafunzo ya kuimarisha kilimo chao. (Photo caption-Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amesema kuwa tayari kandarasi ya ujenzi wa kiwanda hicho imetangazwa)