Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima wa pareto kutoka Nyandarua, Laikipia na Nakuru chini ya muungano wa Aberdares Pyrethrum Caucus, wamemwandikia Rais Uhuru Kenyatta barua wakiitaka serikali kuingilia kati na kuokoa sekta ya pareto, wanayosema imefifia.

Wakizungumza mjini Nakuru siku ya Ijumaa, wakulima hao walisema kuwa idadi ya madeni ya wakulima ni ya kiwango cha juu huku wakimtaka rais kuingilia kati ili wakulima hao waweze kupata haki zao.

“Nimelima pareto kwa miaka mingi, na nimekuwa nikipanda mmea huo kwa wingi. Hata hivyo, siku hizi imebidi nipunguze ekari za mmea huo maanake hakuna malipo. Kama wakulima wa pareto hatutaki mengi kutoka kwa serikali, ila tu tunataka malipo mazuri,” alisema Bw Okindo, mkulima wa pareto.

Wakulima hao wametishia kukosa kutoa mchango wao wa kupiga kura ifikapo kinyanganyiro cha 2017, wakisema kuwa hawatachezewa mchezo wa paka na panya, kama ilivyofanyika kwa wakulima wa miwa.

Wakulima hao walisema kuwa waliohusika na kufuja pesa zao sharti wachukuliwe hatua za kisheria.