Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima wa majani chai katika kaunti ya Nyamira wameshauriwa kuwa waangalifu wanapowachagua wakurugenzi ambao watasimamia viwanda mbalimbali vya mmea huo.

Hii ni baada ya zoezi la upigaji kura ili kuwachagua wakurugenzi hao likiendelea kupangwa huku wakulima wakitakiwa kuwa waangalifu kwa watu watakaowachagua kama wakurugenzi ambao watawapigania kupata haki na kuwanufaisha.

Akizungumza na mwandishi huyu jumatatu, mwenyekiti wa kiwanda cha majani chai cha Sang’anyi wilayani Manga, Richard Migosi alisema watu ambao watachaguliwa kuwa wakurugenzi ni wale ambao watanufaisha wakulima kupata faida kupitia mazao yao bali si wale watarudisha bei ya majani chai  chini bila kujali maslai ya wakulima.

“Mipango ya kura ili kuwachagua wakurugenzi katika kaunti ya Nyamira inaendelea kuratibiwa na tarehe halisi itatolewa. Ninawaomba wakulima wa kuwa makini ili wachague wakurugenzi ambao watawatetea kupata faidi kutoka kwa mazao yao,” alisema Migosi.

Kulingana na mwenyekiti huyo, lengo lake ni kuhakikisha kuwa wakulima wa majani chai wamepata faida inayostahili kutoka kwa mumea wao ndio maana anaendelea kupigania wakulima hao.

“Tunahitaji kuwa na wakurugenzi ambao watapigania wakulima kupata pesa za bonasi ya juu ikilinganishwa na sasa hivi, wale wa kuhakikisha majani yanatolewa kwa vituo kwa wakati unaofaa, kutengeneza barabara zinazoelekea kwa vituo vya ununuzi,” aliongeza Migosi.