Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima kutoka North-Rift wamehakikishiwa kwamba hakutakuwa na upungufu wa mbegu na pembejeo nyingine za kilimo msimu huu wa upanzi.

Kampuni ya mbegu ya Kenya Seed ilisema kinyume na miaka ya awali ambapo wakulima husika wamekuwa wakishuhudia uhaba wa mbegu na mbolea kampuni hiyo imeweka mikakati ya kutosha kuona kwamba imetosheleza matakwa ya mbegu kwa wakulima.

Kampuni hiyo ilisema kuna mbegu ya kutosha katika maghala na katika maduka ya mawakala wake yote katika eno hilo.

Mwakilishi wa kampuni hiyo mjini Eldoret Abednego Sengwer alisema mbali na kuhakikishia kuwa wakulima wanapata mbegu ya kutosha kampuni hiyo itatumia maonyesho ya kilimo ya Eldoret kuelimisha wakulima kuhusu mbinu za kisasa za kuimarisha uzalishaji wa chakula.

"Kama kampuni tumewekea wakulima mbegu ya kutosha,kuna mbegu ya mahindi ambayo inatoa mazao bora zaidi katika eneo hili mbali na mbegu ya mahindi vile tumewaletea wakulima mbegu murua ya ngano ambayo imefanyiwa utafiti wa hali ya juu na kubainika kwamba ina uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula," alisema Sengwer.

Sengwer alisema kampuni yake inatumia maonyesho ya kilimo ya Eldoret kutoa mafunzo kwa wakulima ili kuona kwamba wanaboresha viwango vya uzalishaji chakula nchini.

Wakati huo huo mwenyekiti wa maonyesho hayo Ratcliff Nangalama alitaka kampuni ya maji ya ELDOWAS kuhakikisha kuwa kuna maji ya kutosha wakati wa huu wa maonyesho.

Nangalama alikosoa kampuni hiyo kwa kuzembea katika majukumu yake ambapo tabia hiyo imewafanya wananchi mjini Eldoret kuendelea kushuhudia uhaba wa maji.