Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakulima wa kahawa katika eneo la Mugirango Kaskazini wamemwomba afisa mkuu wa kilimo kuwasaidia kudhibiti ugonjwa fulani ambao umekuwa ukiwasababishia hasara kubwa.

Wakulima hao walisema kuwa zao la kahawa limekuwa likiathirika pakubwa katika eneo bunge hilo, baada ya ugonjwa huo kuathiri mizizi ya kahawa, hali inayosababisha mimea hiyo kukauka na baadaye kuanguka.

"Sisi wakulima tunaokuza zao la kahawa tumekuwa na shida sana kuhusiana na ugonjwa huu unaoathiri mizizi ya kahawa, inayopelekea kuanguka kwa mimea hiyo kwa muda wa wiki mbili pekee. Tumekuwa tukijaribu kupitia kwa wawakilishi wetu kutafuta usaidizi kutoka kwa taasisi ya utafiti wa kahawa kule Kisii bila mafanikio," alisema msemaji wa kundi hilo Fred Nyabuta.

Wakulima hao aidha waliwaomba maafisa husika kuchukua hatua za haraka kukabiliana na ugonjwa huo, kabla haujaathiri mimea zaidi.

"Tunawasihi maafisa wa kilimo kutoka serikali ya kaunti kutembelea mashamba yetu ili kututafutia suluhu la ugonjwa huu kabla haujasambaa zaidi na kuangamiza mimea yetu. Kahawa ndiyo tunayoitegemea sana kupata mapato yetu na iwapo hali hii itaendelea kushuhudiwa, basi tutapata shida kubwa,” alisema Nyabuta.

Wakulima hao walisema maeneo yanayoathirika ni Ekerenyo, Kegogi, Nyamusi na Magwagwa.