Wakulima wa nafaka kutoka Uasin-Gishu wamelalamikia msongamano mkubwa wa magari ambayo yanawasilisha mahindi katika maghala ya Bodi ya Nafaka na Mazao nchini NCPB.
Wakihutubia wana habari katika bohari la NCPB mjini Eldoret siku ya Jumatano, wakulima hao walisema kutokana na wingi wa mahindi, wamelazimika kukaa kwa foleni ndefu mjini humo kwa zaidi ya majuma mawili wakisubiri kuwasilisha mahindi yao kwa NCPB.
Mwakilishi wa wakulima hao Bw Samuel Ayabei alisema hali hiyo inachangiwa na mipangilio duni katika sekta ya Kilimo haswa kilimo cha nafaka.
“Tumekaa hapa kwa siku 15 hali hii inatulazimu kutumia shilingi 1,000 kwa siku ambapo kufikia sasa kila dereva ametumia zaidi ya shilingi 15,000 ambapo hatujui ni nani ambaye ataturudishia pesa hizo," alisema Bw Ayabei.
"Badala ya kupata faida tunaendelea kupata hasara, maisha ya wakulima Kenya yanazidi kuwa magumu."
Bw Ayabei alidai kuwa mahindi ambayo yaliwasilishwa katika ghala hilo tangu mwaka 2012 yangali katika ghala hilo ambapo imekuwa vigumu kupatikana kwa nafasi ya kuweka mahindi zaidi.
Wakulima hao walidai kuwa kuna wafanyibiashara mabwenyenye ambao wamekodi maghala ya NCPB na kuweka mahindi yao huku wakulima wa matabaka ya chini wakiendelea kuumia.
Wakulima husika wanataka NCPB kufungua vituo zaidi vya kununua mahindi kutoka kwa wakulima ili kupunguza msongamano katika maghala ya NCPB Kaskazini mwa Bonde la Ufa.
Usimamizi wa NCPB ulisema kuwa kila juhudi inafanywa ili kukabiliana na changamoto ya msongamano huo.