Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakulima kutoka North Rift wameitaka serikali kupitia kwa Wizara ya Kilimo kuzindua ujenzi wa kiwanda cha mbolea ambacho kilikisiwa kugharimu shilingi bilioni 90.

Wakulima hao walisema serikali iliahidi kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ungeanza mapema mwaka huu walakini kufikia sasa ujenzi huo bado hauajanza.

Kulingana na wakulima hao ni kwamba huenda kuna njama ya kubadilisha mahali ambako kiwanda hicho kilipaswa kujengwa.

Wakiongozwa na mkurugenzi wa Shirikisho la wakulima nchini KFA Bw Kipkorir arap Menjo wakulima hao walisema kuna uvumi kwamba huenda kiwanda hicho kikahamishiwa hadi aidha Thika au Athi River.

Bw Menjo aliitaka serikali kuweka wazi mipango husika ili wakulima wafahamu kinachoendelea.

Hivi maajuzi Naibu Raisi William Ruto akihutubu katika eneo la Kiplombe mjini Eldoret aliwaambia wakulima kwamba tayari mkataba wa maelewano kati ya kampuni ya Toyota Tsusho kutoka Japan na serikali ya Kenya umekamilika kuhusiana na ujenzi wa kiwanda hicho.

"Iwapo ujenzi wa kiwanda hicho utafaulu na kukamilika, masaibu ya wakulima kuhusiana na uhaba wa mbolea mara kwa mara msimu wa upanzi yatakabiliwa," alisema Bw Menjo.

Kwa sasa wakulima hao wanataka serikali kujitolea mhanga na kuona kwamba ahadi hiyo imetimia ikizingatiwa kuwa ilikuwa miongoni mwa ajenda ya kampeini ya Jubilee wakati wa kampeini ya uchaguzi mkuu mwaka wa 2013.