Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya walemavu 4,000 katika kaunti ya Uasin-Gishu wamepokea usaidizi wa vifaa spesheli vya kuwasaidia kukabiliana na changamoto ya kutembea na kuendeleza shughuli zao za kila siku.

Walemavu hao pia walipokea ushauri wa kisaikolojia mbali na kupokea mafunzo ya kuanizisha miradi ya kujikimu maishani.

Mafunzo hayo yalilenga kutoa kasumba ya walemavu kuwa watu wa kuombaomba na kuwataka waanzishe miradi ya kujipatia mapato.

Mshirikishi wa shirika la watu ambao wanaishi na ulemavu kanda ya North-Rift Bw Godfrey Makokha alisema afisi yake ilisajili zaidi ya walemavu 8,000 na ambapo takribani walemavu 4,000 walipokea usaidizi zaidi kutoka kwa afisi hiyo.

“Kupitia kwa afisi hii zaidi ya walemavu 8,000 wameweza kusajiliwa katika kaunti hii ambapo nusu yao ambao ni zaidi ya 4,000 wamepokea usaidizi wa viti vya magurudumu na vifaa vingine spesheli vya kuwasaidia kukabiliana na changamoto ambazo wao hukumbananazo,” alisema

Afisa huyo alisema visa vya ubaguzi dhidi ya walemavu vilianza kurudi chini tangu katiba ya mwaka 2010 ianze kutekelezwa.

“Tangu katiba hii iaanze kutekelezwa vilivyo visa vya ubaguzi dhidi ya walemavu vimerudi chini ambapo walemavu wanapata nafasi sawa na wenzao ambao hawana ulemavu kinyume na haapo awali ambapo walikuwa wakibaguliwa zaidi.” aliongeza

Bw Makokha alisema shirika lake linaendelea na kampeini ya kuhamasisha uma kuhusu umuhimu wa kuhusisha walemavu katika shughuli za kila siku.