Watu wanaoishi na ulemavu mjini Mombasa wamelalamikia kile walichokitaja kama kutengwa nyakati za uchaguzi.
Wameitaka tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kuwawekea mazingira yatakayo wawezesha kushiriki haki yao ya kikatiba kama Wakenya wengine.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao John Karanja siku ya Alhamisi, walemavu hao walidai kuwa walipata taabu wakati wa uchaguzi uliopita kwani dawati zote za maafisa wa IEBC zenye majina ya wapiga kura, zilizidi wengine wao kwa urefu na hivyo kuwatatiza kwani hawangeweza kuyaona majina yao vyema.
Walisema kuwa hali hiyo ilisababisha wengine wao kunyimwa fursa ya kushiriki uchaguzi huo.
“Wengine wetu ni wafupi na hatuwezi fikia dawati hizo. Tunaiomba IEBC izingatie suala hili mambo yasiwe tena kama yaliivyokua wakati wa uchaguzi uliopita,” alisema Karanja.
Aidha, walemavu hao wameitaka IEBC kuweka mikakati itakayohakikisha kuwa baadhi yao wasioweza kufika katika vituo vya kujisajili, wanapata vyeti vya kupigia kura ili wasifungiwe kushiriki uchaguzi mkuu ujao.
Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya walemavu 36,000 waliojisajili kama wapiga kura walikosa kushiriki uchaguzi uliopita kutokana na sababu mbalimbali.
Haya yanajiri wakati tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ikiendelea na zoezi la kuwasajili wapiga kora kote nchini.