Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi mteule wa watu wanaoishi na ulemavu katika bunge la Kaunti ya Nakuru Emma Mbugua amewataka walio na ulemavu kwenye kaunti hiyo kujisajili kama wapiga kura huku zoezi hilo likiwa limesalia siku chache kabla ya kukamilika.

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Nakuru siku ya Ijumaa, Mbugua alisisitiza kwamba walio na ulemavu pia wana haki ya kujisajili kama wapiga kura na kupiga kura kama Mkenya yeyote yule.

Aidha, aliwataka Wakenya pia kudumisha amani haswaa wakati huu ambapo Kenya imeanza kushuhudia joto la kisiasa huku uchaguzi mkuu unapokaribia.

“Twendelee kudumisha amani wakati huu ambapo kampeni za uchaguzi mkuu zimeanza na pia tujisajili kama wapiga kura, haswaa wale walio na ulemavu. Nahimiza pia wasio na ulemavu kujiandikisha kama wapiga kura,” alisema Mbugua.

Wakati huo huo, amewahakikishia walio na ulemavu katika kaunti ya Nakuru kwamba mahitaji yao yanashughulikiwa kwenye bunge la kaunti ya Nakuru kupitia upitishaji wa miswada mbalimbali.

“Tuna mswada wa walio na ulemavu ambao umepitishwa na wawakilishi wa wadi katika bunge la Kaunti ya Nakuru ambao unasubiri kutiwa saini na gavana. Ni mswada wa kuwalinda walio na ulemavu na unaitwa mswada wa watu walio na ulemavu. Walio na ulemavu hawatasalia nyuma,”aliongeza Mbugua.