Mwakilishi mteule wa Wadi Emma Mbugua amewaomba watu wenye ulemavu katika kaunti ya Nakuru kujitokeza na kujisajili kama wapiga kura katika vituo vya usajili vilivyoko karibu nao.
Mbugua ameelezea kuwa hatua hiyo itahakikisha watu hao wanapata fursa ya kuchagua viongozi wanaopenda na ambao watajali maslahi yao.
"Ninawaomba watu wote wenye ulemavu kujisajili katika vituo vya usajili wa kura ili wapate nafasi ya kupiga kura kama watu wengine. Ni haki yao ya kuwachagua viongozi wanaopendekeza bila kutengwa ka njia yoyote ile," Mbugua alidokeza.
Mwakilishi huyo mteule ambaye pia anawakilisha watu wenye ulemavu katika kaunti hiyo ameomba watu wanaoishi na ulemavu kuwasaidia katika shughuli hiyo.
Mbugua alikuwa akizungumza katika shule ya upili ya Ngara ya watu walemavu iliyoko Nakuru ambapo shughuli ya kusajili watu walemavu ilikuwa ikiendelea.
Mwakilishi huyo mteule pia amedokeza kuwa kama viongozi tayari wamepitisha mswada wa kusaidia watu walemavu ambayo itawafaa sana watu hao.
"Ninawasihi watu wenye ulemavu ambao bado hawajapata vitambulisho vya taifa kuhakikisha wameendea vitambulisho vyao ili wapate fursa ya kujisajili kama wapiga kura. Kama viongozi tayari tumepitisha mswada wa kufadhili watu wenye ulemavu katika kaunti hii ambayo itasaidia kuimarisha maisha yao," Mbugua aliongeza.
Kwa upande wake, mwalimu mkuu wa shule hiyo John Gachiga amesifia heshima ya wanafunzi hao huku akielezea kuwa watu hao pia wana haki ya kupiga kura kama wengine.