Baadhi ya walimu Mombasa wamejitokeza kupongeza hatua ya Tume ya kuajiri walimu nchini TSC, kukubali kuwapa walimu marupurupu.
Kulingana na mwalimu mkuu wa shule moja mjini Mombasa aliyezungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano kwa sharti la kutotajwa, hatua hiyo huenda ikaleta suluhu la kudumu kwa mgogoro baina ya walimu na TSC, kuhusu nyongeza ya mshahara ambayo mara nyingi hulemaza shughuli za elimu nchini, hususan nyakati mtihani unapokaribia.
Aidha, mwalimu huyo mkuu alisema kuwa wakati umefika kwa tume ya huduma kwa walimu nchini kulitimiza agizo la mahakama, linaloitaka kuitekeleza nyogeza hiyo kikamilifu ili kuuzuia mgomo wa walimu kutokea tena.
"Tumechoka kugoma kila wakati kwa jambo linanoweza kuzuiliwa. Wakati umefika suluhu ya kudumu iafikiwe ili watoto wetu wasihangaike tena kutokana na mgomo wa walimu,” alisema mwalimu huyo mkuu.
Siku ya Jumanne, TSC ilithibitisha kuwapa walimu nyongeza ya marupurupu itakayohakikisha kuwa mwalimu anayepokea mshahara wa juu atapata nyongeza ya shilingi 10,000, huku wa kiwango cha chini akipokea shilingi 4,000.
Katika taarifa yake, TSC ilisema kuwa hatua hiyo iliafikiwa baada ya kuandaa mazungumzo ya kina na tume ya kuratibu mshahara wa wafanyikazi nchini SRC.