Zaidi ya walimu wakuu 100 wa shule za msingi katika Kaunti ya Mombasa wametia saini mkataba wa kandarasi ya utendekazi ili kuboresha viwango vya elimu.
Mkurugenzi mkuu wa Tume ya kuajiri walimu nchini katika Kaunti ya Mombasa Ibrahim Rugut amesema kuwa mpango huo haulengi kuwakandamiza walimu wakuu bali kuhakikisha kuwa uwajibikaji wa kazi katika shule hizo za umma unatekelezwa vyema.
Akiongea na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatano baada ya kuhudhuria kongamano la walimu wakuu wa shule za msingi za umma, Rugut alisema kuwa walimu wakuu wataendeleza mpango huo kwa walimu wengine ili kuhakikisha kuwa sekta ya elimu inaangaziwa vyema.
“Tunaimani walimu wakuu wa shule za msingi watawaelimisha wenzao na kukubali kutia saini kandarasi hii kwani itawawezesha kutambua utendakazi wao na kupandishwa vyeo,” alisema Rugut.
Wakati huo huo, amewaonya viongozi wa chama cha kutetea maslahi ya walimu Knut na Kuppet kutowapotosha walimu na badala yake kuwashinikiza walimu kukubali mpango huo kwani ndio utakaowawezesha baadhi yao kupandishwa vyeo kutokana na utendakazi wao.
“Tunawaambia viongozi wa Knut na Kuppet kukoma kuwahadaa walimu kususia mpango huu kwani una manufaa makubwa kwa walimu na tunawaomba walimu wapuuzilie mbali shinikizo za viongozi hao,” aliongeza Rugut.
Awali, mpang huo ulikosolewa na viongozi wa kisiasa na wale wa kutetea maslahi ya walimu nchini waliodai kuwa mpango huo wa kutia saini mkataba wa kandarasi ya utendakazi utawakandamiza walimu hao.