Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku masomo katika muhula wa kwanza yakiendelea, waalimu wakuu katika shule za umma wameonywa vikali dhidi ya kuongeza karo ya shule zaidi ya kiwango kilichotolewa na wizara ya elimu nchini.

Wizara ya elimu imesema kuwa tabia hii imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu na kuongeza kwamba waalimu watakaopatikana na hatia hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Haya yamesemwa na naibu mkurugenzi mkuu wa elimu Bi Joy Kelemba alipokuwa akihutubia wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu.

“Lazima kile kiwango cha pesa kilichotajwa na wizara ya elimu kizingatiwe vilivyo na waalimu watakaokiuka agizo hilo tutawafuatilia kwa makini,” alisema Kelemba.

Afisa huyo wa elimu pia amewaomba wazazi wenye ushahidi wa kuonyesha waalimu wakuu wanaoendeleza uovu huo waripoti katika idara husika ili wachunguzwe.

“Kulingana na katiba yetu, mwalimu yeyote anayekiuka agizo hilo anafaa kushtakiwa na tunawasihi wazazi watakaoshuhudia visa hivi watembelee ofisi za elimu na kuripoti mara moja,” aliongezea.

Kelemba alikuwa akiongea hayo katika shule ya Coast Girls mjini Mombasa siku ya Jumatatu, wakati wa zoezi la kuchagua wanafunzi bora watakaojiunga na kidato cha kwanza katika shule za ukanda wa Pwani.

Kwenye agizo hilo la karo katika shule za upili, shule za bweni zinatakiwa kulipisha Shilingi 54, 554 kwa mwaka, huku zile za siku zikitakiwa kulipisha shilingi 9, 374.

Waalimu wakuu kutoka shule mbalimbali ukanda wa Pwani walihudhuria kongamano hilo ambapo walipata fursa ya kuchagua wanafunzi bora watakaojiunga na shule zao wakati zoezi la kusajili wanafunzi litakapoanza hapo January.