Kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni kaunti ya Mombasa Maxwell Masai alisema kuwa walimu wali0husika katika kuwashawishi wanafunzi kushiriki udanganyifu katika wa mitihani ya kitaifa KCSE wachukuliwe hatua za kisheria.
Kulingana Masai, walimu hao ndio wameharibu ndoto za wanafunzi walikosa kupata matokeo yao kutokana na udanganyifu huo na hatua hiyo huenda ikadidimiza sekta ya elimu nchini kufuatia walimu wenyewe kuchangia udanganyifu.
Akizungumza katika eneo la Kisauni mjini Mombasa, Masai alisema kuwa iwapo idara ya elimu kaunti ya Mombasa na wizara ya elimu nchini inalenga kuimarisha viwango vya elimu nchini basi walimu wanaochangia kuzoroto kwa sekta hiyo wanafaa kukabiliwa kisheria.
“Tunaitaka wizara ya elimu kuhakikisha kuwa inawachukulia hatua kali za kisheria walimu wanaodaiwa kuhusika katika kuwashawishi wanafunzi kushiriki udanganyifu wa mitihani," alisema Masai.
"Kwani hali hiyo huenda ikadidimiza kabisa sekta ya elimu nchini,” aliongeza Masai.
Baraza la mitihani nchini KNEC limesema kuwa litaidhinisha sheria kali zaidi zitakazowakabili walimu na wanafunzi wanaoshiriki udanganyifu wa mitihani ya kitaifa nchini ili kuona kuwa elimu inapewa kipau mbele nchini.