Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya wahudumu wa bodaboda 100 Alhamisi walifanya maandamano mjini Nakuru wakishtumu kile wanadai kuwa kuhangaishwa kwa kuitishwa hongo na maafisa wa polisi mjini humo.

Maandamo hayo yametajwa kushinikizwa na mmoja wao baada ya kuumizwa na polisi na pikipiki yake kuharibiwa katika jitihada za kuwatoroka katika eneo la Free Area viungani mwa mji wa Nakuru.

Aidha mhudumu huyo alipelekwa katika hospitali kuu ya jimbo la Nakuru anakoendelea kupokea matibabu.

Mhudumu mmoja wa bodaboda aliyetambulika kama Isaac Mukundi amesema maafisa wa polisi hususan kutoka kituo cha polisi cha Hyrax huwahangaisha kila kuchao hata baada yao kuafikia matakwa yote yanayohitajika kwa mujibu wa sheria zao.

“Nimewahi kupitia kwa hiki kituo cha Medyhill na hata hiki si kituo cha polisi maanake walinichapa na nikanyanganywa kila kitu na nilikuwa na kila kitu, cheti cha usafiri, kofia maalum yote nilikuwa navyo,” alisema Mukundi.

Hata hivyo MCA wa Menengai Michael Macharia ameshtumu kisa hicho na kusema kuwa ameyaripoti malalamishi ya wahudumu hao kwa OCPD wa Nakuru Musa Kongoli ambaye kwa sasa anaendeleza uchunguzi.

Wakati uo huo amewataka wanabodaboda hao kuzingatia sheria zote za wahudumu ili kuzuia visa vya kugongana na maafisa hao.