Wanachama wa vuguvugu la Mombasa Republican wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika usajili wa wapiga kura ilikuhakikisha mageuzi ya haraka ya uongozi wa nchi hii yanapatikana.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alisema kwamba hiyo ndio njia pekee ya kuibandua serikali ya Jubilee mamlakani, aliyoitaja kama ya ubepari na ufisadi.
Akiwahutubia wananchi wa Kwale siku ya Jumapili, Kalonzo aliwahimiza wanachama wa baraza hilo kujitokeza na kujisajili kama wapiga kura kwa mujibu wa katiba.
Aidha, hakusita kwa kuikashifu serikali ya Jubilee, akisema kwamba imeshindwa kutimiza ahadi kwa wakenya na badala yake inaendeleza ufujaji wa fedha za umma na kuendeleza ufisadi.
Hatua hii inajiri baada ya kuenea tetesi kuwa wafuasi wa MRC hawatapiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka 2017.
Hii ni kutokana na misimamo mikali ya vuguvugu hilo linalodai kuwa 'Pwani si Kenya'.