Wanafunzi 140 kutoka familia maskini katika kaunti ya Nyamira wamefadhiliwa pesa za basari kupitia hazina ya 'Affirmative Social Development Fund' ili kujiendeleza kielimu.
Akizungumza mjini Nyamira alipotoa pesa hizo, mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Nyamira Alice Chae alisema atahakikisha wanafunzi hao wamepata fursa ya kumaliza masomo yao ili nao waweze kujiimarisha kimaisha.
Chae alisema kuwa wanafunzi ambao walikabidhiwa pesa hizo ni wa shule za upili mbalimbali na vyuo vya kati, huku akiongeza kuwa hazina hiyo haiwezi kutoa pesa hizo kwa wanafunzi wa shule za msingi na wa vyuo vikuu.
Wanafunzi hao walipokezwa kati ya shillingi 4,000 hadi 7,000 kila mmoja, kulingana na kiwango cha shule cha mwanafunzi husika.
Aidha, Chae alipongeza serikali kwa kuanzisha hazina hiyo ambayo imeanza kutoa usaidizi katika kaunti ya Nyamira na kusema kuwa hazina hiyo itafanya mengi.
“Napongeza serikali ya kitaifa kwa kuleta hazina hii na tutaendelea kufanya mengi kwa kufadhili masomo ya wanafunzi hawa maana kuna wengine ambao hawajiwezi kabisa,”alisema Chae.