Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi wanaosomea taaluma za juu katika vyuo vikuu nchini wametakiwa kujitenga na maswala ya ugaidi na itikadi kali.

Akizungumza wakati wa matayarisho ya uchaguzi wa Muungano wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi tawi la Mombasa siku ya Ijumaa, mwenyekiti wa wanafunzi chuoni humo Mohammed Kalmey alisema kwamba wanafunzi katika vyuo vikuu wanashawishiwa kifedha ili kujiunga na kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Kalmey alisema kwamba wanafunzi hao sasa wamechukua jukumu la kuhamasishana kuhusu athari za misimamo mikali na ugaidi kwani swala hilo limeathiri vijana na wanafunzi wengi humu nchini.

“Tumechukua jukumu la kuelimishana jinsi ya kuepukana na vishawishi kutoka kwa wafuasi wa al-Shabaab kwani wanalenga sana wanafunzi wa taalum za juu katika vyuo vikuu. Sisi tungependa sana taifa letu kuwa la amani,” alisema Kalmey.

Mwenyekiti huyo wa wanafunzi aidha aliwahimiza viongozi wa kidini kutowatenga wanafunzi hao na badala yake kuwashauri na kuwaelekeza vyema kwa ajili ya msingi bora.

Kauli ya kiongozi huyo wa wanafunzi imejiri baada ya ripoti za polisi kuashiria kwamba wanafunzi wa vyuo vikuu wanalengwa na kundi la kigaidi la al-Shabaab.