Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku likizo ya Desemba ikisherehekewa kwa njia mbali mbali na watu wa ngazi tofauti, baadhi ya wanafunzi wamesalia kufanya marudio na kujishughulisha na masomo ya ziada.

Idadi ya kuridhisha ya wanafunzi ilionekana kuzagaa katika ukumbi wa maktaba ya kitaifa ya Mombasa kinyume na matarajio ya wengi, angalau kuziba ufa ulioachwa na mgomo wa walimu.

Kulingana na mhudumu mkuu katika maktaba hiyo ya Mombasa Augustine Mutiso, idadi hiyo ni maradufu ikilinganishwa na mwaka uliopita haswa katika kipindi hiki cha likizo ya mwezi Desemba.

“Ni nadra sana kupokea idadi kubwa ya wanafunzi wanaokuja kudurusu katika nyakati hizi za likizo ya mwisho wa mwaka, kwani wengi wao aidha wamesafiri au wanajishughulisha na michezo mbali mbali,” alinakili Mutiso.

Kwa upande wa baadhi ya wanafunzi walikuwa katika maktaba hiyo ya Mombasa, yao ni kuhakikisha wanapunguza mwanya ulioachwa na walimu wakati walipokuwa katika mgomo wa kitaifa wakidai nyongeza ya mishahara wao kwa asilimia 50 hadi 60.

Hata hivyo, mhudumu huyo amesisitiza kuwa ni jambo la kutiliwa mkazo kuona kuwa wanafunzi wanatumia wakati wao vyema katika kipindi hiki cha likizo, ili kuona kuwa hawapotezi waliyoyasoma mbeleni sawia na kuimarisha viwango vya matokeo yao watakapofungua shule kwa muhula wa kwanza.

Vile vile, amewataka wazazi kuwa karibu sana na wana wao katika kutambua harakati zao ili kuwatahadharisha na matumizi ya mihadarati sawia na kujihusisha na vikundi vya uhalifu.