Mwakilishi wa Wadi ya Bogichora Beauttah Omanga amewaomba wanakandarasi wanaokabidhiwa kandarasi katika Kaunti ya Nyamira kukamilisha miradi hiyo kwa muda unaofaa.
Omanga alisema baadhi ya wanakandarasi hupewa kandarasi na kufanya poleple hadi mwaka unaofuata kufika kabla ya kukamilisha kandarasi hizo, jambo ambalo alisema si halali.
Akizungumza siku ya Jumatano katika wadi ya Bogichora, Omanga alilalamikia ujenzi wa daraja la Riabima ambalo liko katika wadi hiyo, kwa kusema kuwa tangu mwanakandarasi kukabidhiwa kazi hyo mwezi mmoja uliopita, bado hakuna dalili za ujenzi huo kuanza.
Omanga alimwomba mwankandarasi aliyepewa kazi ya kukarabati daraja hilo kuanzisha ujenzi huo ili wakazi waweze kupata mahala pa kupita.
“Ikiwa mwanakandarasi ameshindwa kufanya kazi, anastahili kusema mapema ili mwanakandarasi mwingine kutafutwa. Hakuna haja ya kusubiri kitu ilhali huoni matunda yake,” Omanga
Aliongeza, “Naomba mwanakandarasi aliyepewa kazi ya kukarabati soko hili kukamilisha ujenzi huo haraka, na kama hayuko tayari kufanya kazi hiyo, aseme ili mwanakandarasi mwingine atafutwe,” alisema Omanga.
Aidha, aliomba serikali kuwachunguza wanakandarasi ambao hupewa kazi hizo kabla ya kuwapokeza kandarasi hizo, kwani wengi hufanya kazi polepole na kupelekea miradi mingi kutokamilika kwa muda unaofaa.
“Sisi sote sharti tuwajibike katika kazi ambayo tunayoifanya katika serikali yetu, ili kuhakikisha maendeleo yamefanywa katika sehemu zote za kaunti,” alisema Omanga.