Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa barabara na kazi za umma katika serikali ya kaunti ya Nyamira amewaonya vikali wanakandarasi wanaokarabati barabara bila kuafikia viwango vinavyohitajika. 

Akihutubia wanahabari siku ya Jumapili wakati wa ukaguzi wa barabara zinazoendelea kukarabatiwa mjini Nyamira, Komenda alisema wizara yake haitasita kuwaondoa kwenye sajili wanakandarasi walio na mazoea yakufanya kazi duni. 

"Wakazi wa Nyamira wanataka kuona ukarabati wa barabara ukifanywa kwa haraka na kwa njia inayofaa, na kwa maana hiyo wale wanakandarasi wanaofikiria kwamba wizara itaketi tu na kuangalia wakifanya kazi duni wacha wajue kuwa watachukuliwa hatua za kinidhamu," alisema Komenda. 

Komenda aidha alihisihi kampuni ya usambazaji nguvu za umeme nchini KPLC kuondoa vikingi vya stima vilivyoko kwenye sehemu za barabara zinazokarabatiwa kama njia mojawapo ya kuwarahisishia wanakandarasi kazi. 

"Ombi langu kwa kampuni ya Kenya Power ni kuondoa vikingi vilivyoko kando kando mwa barabara zinazokarabatiwa ili kurahisishia wanakandarasi kazi na pia kupunguza visa vya ajali," aliongezea Komenda.