Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba amemkosoa mwanakandarasi anayeendeleza ujenzi wa barabara ya Mtopanga-Bamburi kwa kuchelewesha ujenzi wa barabara hiyo.

Kulingana na mbunge huyo hali hiyo imesambaratisha shughuli za uchukuzi katika barabara hiyo huku biashara nyingi zikiathirika pakubwa.

Akizungumza katika eneo la Kisauni siku ya Jumatano, baada ya kukagua miradi ya kimandeleo, Bedzimba alisema kwamba wanakandarasi kama hao wanapaswa kunyang’anywa kandarasi hizo na kupewa watu wengine walio na uwezo wa kuitekeleza kazi hiyo vyema.

Bedzimba alilitaja eneo hilo la Kisauni kama eneo linalokumbwa na changamoto katika hali ya miundo msingi na kama viongozi wa eneo hilo, wamejitahidi mno ili kuona kwamba hali ya miundo msingi katika eneo bunge hilo inaimarishwa.

“Wale wanakandarasi wasiowajibikia majukumu yao na kutekeleza kazi zao watatimuliwa. Hatuwezi kuruhusu watu kuzembea katika kazi zao na wananchi wanahitaji kutekelezewa maendeleo,” alisema Bedzimba.

Kauli ya Bedzimba inajiri huku wakazi wa maeneo ya Bokole, Bomu na Mwagosi katika eneo bunge la Changamwe wakilalamikia hali duni ya miundo msingi ambayo imechangia katika kushuhudiwa mafuriko.