Kamati ya mazingira katika Kaunti ya Mombasa imesema kuwa yeyote atakayepatikana akitupa taka kiholela atatozwa faini au kutumikia kifungo gerezani.
Kamati hiyo imesema kuwa imeweka mikakati maalum ya kuboresha usafi wa jiji ambapo atakayepatikana na hatia hiyo atatozwa takribani shilingi 100,000 au kifungo cha miaka sita gerezani.
Akizungumza katika kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, kaimu Mkuu wa Idara ya Maji na Mazingira Tendai Lewa, alisema kuwa hatua hiyo ni njia moja ya kuhakikisha kuwa wanaweka usafi wakati huu ambapo wageni wengi wanazuru eneo hilo.
“Mji wetu sasa hivi unapokea wageni wengi na tunafaa kushirikiana kuhakikisha kuwa tunadumisha usafi wa hali ya juu,” alisema Lewa.
Kamati hiyo ilisema kuwa changamoto kubwa wanayopitia ni kuwa baadhi ya wakaazi huharibu pipa za taka zinapowekwa katika maeneo ya makazi.
Aidha, Lewa alisema kuwa kuna nambari maalum ya simu ambayo wataitoa kwa umma na kuongeza kuwa wakaazi wanafaa kuchukua fursa ya mitandao ya kijamii kuripoti mtu yeyote atakaye kukiuka sheria hiyo.
Kamati hiyo pia imesema imeajiri zaidi ya wafanyikazi 40 watakaoendeleza shughuli ya usafi wa mji, pamoja na maafisa kadhaa watakozunguka wakihakikisha kuwa hakuna mtu anayetupa taka ovyo.