Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanasiasa wanaoendeleza siasa za chuki na matamshi ya uchochezi wameonywa kusitisha matamshi hayo la sivyo watakabiliwa kisheria na maafisa wa usalama.

Naibu Kamishna wa kaunti ya Mombasa Mahamoud Salim amesema kuwa kuendelea kukithiri kwa matamshi ya chuki na uchochezi katika mikutano ya hadhara huenda ukawagawanya wakenya na kuzua malumbano.

Kwenye mahojiano ya kipekee na mwanahabari huyu mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mahamoud alisema kuwa maafisa wa usalama wametumwa nyanjani kuwa chunguza viongozi wanaowachochea wakazi kuzua vurugu kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa, akisema kuwa mikutano ya hadhara inafaa kuwa ya amani.

"Tunawaonya wanasiasa wanaoendeleza matamshi ya chuki na uchochezi katika mikutano ya hadhara kukoma mara moja na kueneza ujumbe wa amani na iwapo hawatazingatia hilo basi maafisa wa usalama watawakabili kisheria,” alieleza Mahamoud.

Wakati uo huo, amewataka wakazi wa kaunti ya Mombasa kushirikiana na maafisa wa usalama katika kukabiliana na changamoto za kiusalama ili kaunti hiyo kuwa salama.

Hatua ya afisa huyo tawala imejiri huku mchakato wa kisiasa katika kaunti hiyo ukianza rasmi na kuzua taharuki miongoni mwa jamii.