Wanasiasa wote nchini wameombwa kutoeneza siasa za ukabila, na bkuendesha siasa za kuwaunganisha wakenya pamoja ili kuleta maendeleo.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano mjini Kisii, mwenyekiti wa chama cha Kenya National Congress Atati Kengere alisema wakenya wote wanastahili kuunganishwa na wanasiasa bila kujali misingi ya ukabila ili maendeleo kuhakikishwa kote nchini.
Kulingana na mwenyekiti huyo, siasa za ukabila hugawa wakenya na kupelekea maendeleo na uchumi wa taifa kudidimia kwani hayo yote hurudishwa nyuma wakati hakuna umoja.
“Kila mwanasiasa apige siasa za kuunganisha wananchi ili sote tufaidike na maendeleo, na uchumi wa taifa uweze kuinuka zaidi,” alisema Kengere.
Aidha, Kengere aliomba jamii ya mkisii kutojihusisha kwa masuala ya ukabila kwani umoja ni nguvu haswa wakati wa kutafuta uongozi.
Ata hivyo, Kengere aliomba serikali ya kitaifa kutimiza ahadi ilizotoa wakati wa kampeini katika eneo la Kisii.
"Naomba serikali kujaribu kila iwezalo kuhakikisha maendeleo yameanzishwa na kukamilishwa katika eneo la Kisii," aliongeza mwanasiasa huyo.