Viongozi wa kisiasa humu nchini wameonywa dhidi ya kutoa matamshi ya chuki na uchochezi ili kuzuia kuwagawanya Wakenya katika misngi ya kisiasa na kikabila.
Akiwahutubia wakazi mjini Malindi, Mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga amewashauri wanasiasa wanaotafuta kiti cha ubunge wa Malindi kuwa na hekima wakati wanapoendeleza kampeni zao za kisiasa ili kuwaunganisha Wakenya pamoja na kudumisha amani.
Gunga amesema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wameanza kufanya mikutano ya kisiri ya kikabila mjini Malindi hali ambayo ameitaka kuwa huenda ikaleta uhasama.
“Ninawashauri viongozi wa kisiasa kutumia hekima wakati wanapohutubia mikutano ya kisiasa ili kuzuia kuwagonganisha Wakenya kwa misingi ya kisiasa na kikabila hilo halitakuwa jambo jema katika taifa hili,” alisema Gunga siku Jumamosi katika mkutano wa kisiasa.
Gunga ameyasema hayo wakati alipokuwa akiendeleza kampeni za kumpigia debe mgombea wa kiti hicho cha ubunge wa Malindi kupitia chama cha Kadu Asili Reuben Katana.
Uchaguzi huo mdogo wa kuwania kiti cha ubunge wa Malindi kilichowachwa na Dan Kazungu aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Madini nchini umepangwa kufanyika tarehe saba mwezi Machi mwaka huu.